Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael ametaja sababu ya kumuondoa kambini winga Bernard Morrison muda mchache kabla ya mchezo wa kombe la FA dhidi ya Kagera Sugar ambao ulipigwa uwanja wa Taifa jana
Eymael amesema suala la nyota huyo ameuachia uongozi wa Yanga kuamua kwani pamoja na kuzungumza nae mara kadhaa, ameendelea kuwa 'mtukutu'
"Niliamua kumuondoa kambini baada ya kutoridhishwa na tabia yake. Nimezungumza nae mara kadhaa lakini nasikitika amebadilika sana. Huyu sio Morrison niliyemleta hapa, sifahamu amekumbwa na nini"
"Sitaki kulizungumza zaidi suala lake, nimewaachia viongozi wa Yanga kuamua nini cha kufanya," alisema Eymael
Inaelezwa juzi usiku Morrison alijaribu kutoroka kambini kabla ya kudhibitiwa na Ma Bodigadi wa Yanga ambao alifikia hatua ya kutaka kupigana nao
Ni dhahiri huyu sio aina ya mchezaji ambaye Yanga wanahitaji kuendelea kuwa nae
Huenda Yanga italazimika kuvunja mkataba wake kwa kigezo cha nyota huyo kurudisha gharama zote ambazo GSM wametumia kumleta nchini
Kama sivyo anaweza kukaa 'juu ya mawe' kwa miaka yote miwili ya mkataba wake kwani hata kama akiamua kuondoka, Yanga itaendelea kushikilia ITC yake na hivyo hawezi kuruhusiwa kuitumikia timu yoyote bila ya ITC hiyo