Hivi karibuni Mkurugenzi wa uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said alifichua kukamilika kwa mchakato wa usajili wa wachezaji watatu wa kigeni ambao wanasubiri wakati mwafaka waweze kutambulishwa
Hersi pia akabainisha kuwa wako kwenye mazungumzo ya kumalizana na wachezaji wengine wawili wa kigeni hivyo kufanya idadi ya nyota wapya wa kigeni ambao watasajiliwa na mabingwa hao wa kihistoria kuwa watano
Lakini juzi wakati akizindua Tawi la Yanga huko Musoma, Hersi akafichua kuwa nyota wazawa wanne nao watasajiliwa na hivyo kufanya idadi ya wachezaji wapya ambao watasajiliwa na Yanga kuwa tisa
Hersi alisema GSM wamedhamiria kuirejesha Yanga kwenye makali yake, hilo ni jambo muhimu kwa muktadha wa kibiashara kwani kama timu haitafanya vizuri, hata mauzo ya jezi yatashuka
"GSM ni watu wa mafanikio, hatuna historia ya kufanya jambo likashindwa. Mipango yetu tunaifanya kwa ustadi na ukamilifu"
"Poleni wana Yanga, huu mwaka ulikuwa wa majonzi majonzi ila msimu ujayo utakuwa wa furaha kwetu kwa maana kwanza tunafumua kikosi chetu ambapo tutakiboresha zaidi kwa kusajili wachezaji wa kigeni wa kiwango cha juu watano na wachezaji wa ndani wanne.
"Hatuwezi kuwa katika timu inayofanya ovyo hivyo msimu ujayo msiwe na shaka," alisema