Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo kwa kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa watani zao Simba katika mchezo wa nusu fainali kombe la FA uliopigwa uwanja wa Taifa jana
Eymael amesema vijana wake hawakuwa na mchezo mzuri, walicheza chini ya kiwango
"Sitaki kuzungumza majina , lakini ni wazi leo hatucheza vizuri, nawapongeza wapinzani wetu walikuwa bora. Najua ni matokeo yaliyowaumiza mashabiki wetu lakini tunawaahidi tutarejea tukiwa imara. Nitazungumza na wachezaji wote kwani hata wao matokeo haya yamewaumiza"
"Tunahitaji kumaliza katika nafasi ya pili kwenye ligi, hivyo tunapaswa kuwa sawa kabla ya mchezo wetu unaofuata," alisema Eymael
Aidha Eymael aligoma kuzungumzia tukio lililofanywa na winga Bernard Morrison ambaye aliondoka moja kwa moja uwanjani baada ya kufanyiwa mabadiliko
Yanga itashuka uwanja wa Taifa siku ya Jumatano kuumana na Singida United katika mchezo wa ligi kuu
Mabingwa hao wa kihistoria wamebakia na malengo ya kumaliza katika nafasi ya pili baada ya kuondoshwa kwenye michuano ya kombe la FA, huku pia wakiwa na hatihati ya kukosa ushiriki michuano ya Kimataifa msimu ujao
Kama Yanga itafanikiwa kumaliza kwenye nafasi ya pili katika ligi na Simba ikafanikiwa kutwaa kombe la FA, basi miamba hao watakutana tena katika mchezo wa Ngao ya Jamii