Mshambuliaji wa Yanga Yikpe Gnamien raia wa Ivory Coast, ana mechi tatu tu za kuwashawishi mabosi wa timu hiyo kumjumuisha katika kikosi cha msimu ujao
Baada ya juzi kufunga bao lake la pili kwenye ligi katika mchezo dhidi ya Singida United, kesho Jumamosi atakuwa na nafasi nyingine kwenye mchezo dhidi ya Mwadui Fc
Kisha mechi mbili zitakazobaki ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar na Lipuli Fc
Mshambuliaji huyo aliyetua Yanga usajili wa dirisha dogo akitokea klabu ya Gor Mahia, dalili zote zimeonekana, mkataba wake unaweza kuvunjwa
Hata hivyo kocha mkuu wa Yanga Luc Eymael amesema Yikpe ana mechi tatu za kuthibitisha kuwa anastahili kuendelea kukipiga Yanga
Eymael amesema alivutiwa na upambanaji wake kwenye mchezo dhidi ya Singida United akifunga bao lakini pia akikosa nafasi nyingine mbili za wazi
"Nilimpa nafasi Yikpe kwenye mchezo dhidi ya Singida United, nilihitaji kuongeza kasi katika ushambuliaji, na kwa kiasi kikubwa alifanya kile nilichomuelekeza," alisema Eymael
"Lakini nimemwambia ana mechi nyingine tatu kupigania nafasi yake katika timu, kama atafanya vizuri kwenye michezo hiyo tunaweza kumfikiria. Naamini mchezo wa Singida United utamuhamasisha kufanya vizuri zaidi kwenye mechi zilizosalia"
Yanga inatajwa kuwa mbioni kuisuka upya safu yake ya ushambuliaji ikihusihwa na washambuliaji watatu wa kigeni Heritier Makambo (Horoya AC), Mpiana Monzizi(FC Lupopo) na Yacouba Sogne (Asante Kotoko)