Kuelekea kukamilika kwa msimu wa ligi kuu ya Vodacom, Yanga inakabiliwa na mtihani kupata matokeo katika mechi ngumu ugenini
Siku ya Jumatano, itaanza kwa kuumana na Mtibwa Sugar kisha kuelekea Iringa kuifuata Lipuli Fc kwa ajili ya mchezo wa mwisho ambao utapigwa Jumapili, Julai 26
Ugumu wa michezo hiyo unatokana na mazingira yanayozikabili Mtibwa Sugar na Lipuli ambazo ziko hatarini kuteremka daraja kama hazitashinda mechi zilizobaki
Mtibwa Sugar iko kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa ligi wakiwa katika nafasi ya 14 baada ya kufikisha pointi 41 wakicheza michezo 36 na wanapaswa kushinda michezo miwili iliyosalia
Hali iko hivyo hivyo kwa Lipuli Fc ambao wanashika nafasi ya 15 wakikusanya alama 41, wanatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Mtibwa Sugar
Vilabu vinne vitashuka daraja moja kwa moja msimu huu huku timu nyingine nne zikitarajiwa kucheza Play-off
Kwa upande wa Yanga ni michezo ambayo matokeo ya ushindi ni lazima ili kujihakikishia nafasi ya pili wanayoishikilia sasa
Hii ni michezo ambayo pia itawapa nafasi baadhi ya nyota wa Yanga ambao wako kwenye hatihati ya kutemwa, kumshawishi kwa mara ya mwisho kocha Luc Eymael
Yanga ina mkakati wa kukiimarisha kikosi chake, zoezi ambalo litashika kasi pale ligi itakapomalizika mwishoni mwa wiki hii