Aliyewahi kuwa kocha Mkuu wa Yanga Hans van Der Pluijm amesema hana kinyongo kurejea kuwanoa mabingwa hao wa kihistoria kama viongozi watamkabidhi majukumu hayo
Pluijm ambaye kwa sasa yuko mapumziko nyumbani kwake Ghana, amesema anaifahamu vyema Yanga pamoja na soka la Tanzania, akiwataka viongozi wafanye maamuzi mapema ili wawah muda wa maandalizi kuelekea msimu ujao
"Uamuzi uko mikononi mwa uongozi, wao ndio wanajua wanataka klabu yao iende wapi, wanatakiwa kuwa makini kama wanataka mataji, hakuna kubahatisha," alisema Pluijm.
Pluijm amesema Yanga inatakiwa kuanza mapema maandalizi ya msimu ujao kwa sababu muda uliobakia kuelekea msimu mpya ni mdogo
"Mpira wa miguu unachezwa hadharani, hauhitaji majaribio au miujiza, ni lazima maandalizi sahihi yafanyike, ukifanya hivyo, utatarajia matokeo mazuri, usipofanya, usitarajie makombe, itakuwa ngumu," alisema kocha huyo.
Aidha, Mholanzi huyo aliweka wazi kwa sasa yuko huru, hana timu na anafanya shughuli zake binafsi kwenye makazi yake nchini Ghana.
"Sina timu, niko huru, nimepata salamu za kutakiwa lakini si rasmi, kama tutazungumza na viongozi na kufikia makubaliano, nitakuwa tayari kuja tena Tanzania, maisha ya mpira ni ya kuzunguka, unaweza kwenda mbali au ukarudi kule ulikotoka, kikubwa ni kuweka alama nzuri kila unapofanya kazi," aliongeza
Pluijm anaongoza orodha ya makocha wanaotajwa kumrithi Luc Eymael aliyetimuliwa hivi karibuni
Mshindani wake wa karibu ni kocha wa zamani wa Simba Patrick Aussems huku jina la Mwinyi Zahera aliyeondolewa mwanzoni mwa msimuΒ huu uliomalizika nalo likichomoza
Kamati ya ufundi Yanga inaendelea kupitia maombi yaliyowasilishwa na makocha zaidi ya 62 ili kumpata mmoja atakayepewa jukumu la kuisuka upya Yanga