Baada ya nahodha wa Yanga Papy Tshishimbi kusuasua kusaini mkataba mpya, mambo yamemgeukia kwani Yanga ni kama wamemfungia 'vioo' baada ya kuamua kusajili wachezaji wengine katika nafasi yake
Zilianza kama tetesi lakini sasa kuna uhakika mkubwa kiungo mkabaji kutoka AS Vita Mukoko Tonombe anaweza kutua kuchukua nafasi yake
Lakini pia za chinichini ni kuwa Yanga imetua pale Kagera Sugar ikihitaji saini za viungo wawili walioibeba timu hiyo msimu uliomalizika, Zawadi Mauya na Awesu Awesu
Mauya ni kiungo mkabaji, mtu wa kazi kwelikweli, kama Yanga watafanikiwa kumnasa, ni wazi Tshishimbi hatakuwa na nafasi kwenye kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria
Tshishimbi atajilaumu mwenyewe kwani alipewa mkataba tangu mwezi March lakini akasuasua kuusaini ikielezwa anataka fedha zaidi
Yanga inayosukwa sasa siyo ya kubembeleza wachezaji, inaelezwa wachezaji wanapewa ofa kulingana na mchango na kiwango chao katika msimu uliomalizika
Kwa wale ambao watagomea ofa hizo, wataruhusiwa kuondoka ili nafasi zao wasajiliwe wachezaji bora zaidi yao