Uongozi wa klabu ya Yanga umesema hauridhishwi, na hukumu iliyotolewa kwenye shauri la Morrison watakwenda Mamlaka za juu kuitafuta haki
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Dk Mshindo Msolla amesema wamevumilia matukio mengi ya dhurma ambayo wamefanyiwa lakini hili hawatakubali
Dk Msolla amehoji kitendo cha Morrison kwenda kusaini mkataba na klabu ya Simba na wakati huohuo akiwa na kesi ya kimkataba na Yanga
Lakini pia ni kitendo cha mchezaji huyo kumshukuru Zacharia Hans Poppe kwa kufanikisha usajili wake
Hans Poppe ni Mjumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, Yanga ilipinga uhalali wake wa kushiriki shauri hilo lakini TFF walimkingia kifua
"Kuna vitendo vingi ambavyo vinafanywa na TFF Yanga hairidhishwi navyo. Mchezaji anawezaje kusaini mkataba wakati ana kesi ya Kimkataba? Haitoshi anamtaja na kiongozi wa Kamati aliyemsajili lakini bado hatua hazichukuliwi? Huu ni mpira au upuuzi, " alihoji Dk Msolla
"Mpira wa Tanzania tunapaswa kuacha ujanja ujanja ili tuweze kuendelea. Haiwezekani TFF iteue kiongozi kutoka timu fulani kusimamia kesi ya timu pinzani mmeona wapi? Mchezaji anamshukuru kuongozi flani kwa kumsajili halafu kiongozi huyohuyo anaingia kwenye kamati ya Maamuzu dhidi yetu?"
"Tunajua lengo ni kutufedhehesha viongozi wa Yanga kwa mashabiki zetu pamoja na kumfedhehesha Mdhamini wetu GSM lakini tunawaambia Wanachama wa Yanga tuko imara, hatutakubali kuyumbishwa"
Klabu ya Yanga imesisitiza kusubiri nakala ya hukumu ya shauri hilo ili waweze kwenda Mamlaka za juu na hawako tayari kuomba 'review' ya hukumu kutoka kwa watu wale wale ambao wametoa hukumu