Ukweli ni kwamba kwa usajili ambao Yanga imefanya, matumaini ni makubwa ile dhamira ya kuurejesha nyumbani ubingwa wa ligi kuu uliopotea kwa misimu mitatu, imeonekana
Ukiangalia wachezaji wote waliosajiliwa na Yanga, unaweza kubashiri nini kinaenda kutokea msimu ujao
Yanga imesajili wachezaji wenye uwezo wa juu, nyota ambao hawatahitaji muda mrefu sana kuweza kuelewana
Hawa wachezaji wote wanaokuja sio wa majaribio kama ilivyokuwa msimu uliopita. Safari hii haujafanyika usajili wa bahati nasibu kwani wachezaji wote uwezo wao ulifahamika kabla
Msimu uliopita, kilio cha kila Mwanayanga ilikuwa upande wa safu ya ushambuliaji
Sasa angalia wachezaji waliosajiliwa mpaka sasa kuimarisha eneo hilo, Tuisila Kisinda, Farid Mussa, Waziri Jr, Yacouba Sogne, Michael Sarpong na Carlinhos
Unaweza kuona Yanga inarejesha utamaduni wake wa kushambulia kupitia pembeni kwani imewapata watu wa kazi, Kisinda na Farid
Lakini pale eneo la ushambuliaji kati wapo Waziri, Sarpong na Sogne ambao wote wanaweza kufunga mabao kwa kila namna
Sarpong kwa asili yeye ni namba 10, ana uwezo mkubwa wa kutandika makombora kutoka kila upande
Sogne alishawahi kuja nchini akiwa na klabu ya Asante Kotoko na akawafunga majirani zetu, ni mzuri sana kwenye umaliziaji lakini pia fundi mmoja wa kupiga mipira iliyokufa. Kwa aina ya washambuliaji wa pembeni ambao Yanga imewaleta, Yacouba anaweza kufunga mabao mengi
Waziri huyu ni aina ya Makambo, Wengine wanaweza kubeza usajili wake, lakini kumaliza msimu akiwa amefunga mabao 15 kwenye ligi kuu pamoja na playoff sio jambo dogo
Carlinhos ni fundi, mtaalamu eneo la kiungo. Huyu atanogesha pale kati akishirikiana na akina Haruna Niyonzima, Feisal Salum 'Fei Toto' na Mukoko Tonombe
Wanayanga wasubiri kushangilia tu...!