Mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga wameukaribisha msimu kibabe baada ya kuichapa Aigle Noir mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Mkapa usiku wa leo
Ilikuwa ni siku ya kipekee kwa mashabiki wa Yanga waliojitokeza kwa wingi uwanja wa Mkapa, kwani waliujaza, hapakuwa na sehemu hata ya kutemea mate
Kabla ya mchezo huo kulikuwa na shamra shamra za burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo Harmonize 'Jeshi' aliyeingia uwanjani na kamba
Lakini kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu na mashabiki ni mchezo huo ambao umewapa taswira Wanayanga kuwa wanakwenda kuwa na msimu mzuri
Licha ya wachezaji kuwa pamoja kwa siku chache, Yanga ilikuwa katika kiwango bora, nuda wote mashabiki wakishangilia kandanda lililokuwa likipigwa
Kipindi cha kwanza viungo Mukoko Tonombe na Feisal Salum 'Fei Toto' waliliteka dimba la kati huku Tuisila Kisinda akidhihirisha thamani yake mapema tu kwa kuifungia Yanga bao la kwanza

Walinzi wa pembeni Yassin Mustafa na Kibwana Shomari walionyesha kile ambacho Yanga wamekikosa kwa muda mrefu
Hakika wachezaji hawa wakikaa pamoja kwa angalau mwezi mmoja, hakuna timu itausogelea moto huu wa Yanga
Safu ya usambuliaji iliongozwa na Michael Sarpong akishirikiana na Ditram Nchimbi
Pamoja na kuwa wawili hao waliuanza mchezo taratibu, ushirikiano wao uliisaidia Yanga kufunga bao la pili kwenye kipindi cha pili Sarpong akiitendea haki krosi ya Nchimbi akiifungia Yanga bao la pili kwa kichwa
Katika kipindi cha pili, kocha Mwambusi alibadili nusu ya kikosi kilichoanza akiwaingiza nyota wengine kama Waziri Junior, Haruna Niyonzima, Zawadi Mauya na Farid Mussa
Kasi ya Farid ilikuwa changamoto kwa walinzi wa Aigle Noir, Junior itabidi ajilaumu mwenyewe kwa kutotumia nafasi alizopata
Kiungo Muangola Carlinhos alipewa nafasi kwenye dakika 10 za mwisho nusura aifungie Yanga bao kama sio uhodari wa mlindalango wa Aigle
Huu ni mwanzo mzuri kwa kikosi kipya cha Yanga, kuna kila dalili huu utakuwa msimu wa furaha kwa mashabiki wa Yanga