Kiungo kiraka Deus Kaseke amepewa majukumu ya kukiongoza kikosi cha Yanga msimu huu akiwa nahodha ambaye atasaidiwa na Haruna Niyonzima
Kaseke alimaliza msimu uliopita akiwa miongoni mwa wachezaji bora wa Yanga, amepania kuendeleza pale aipoishia
Aidha, amesema majukumu ya unahodha aliyopewa yatamfanya apambane zaidi ili kuhakikisha anakuwa na nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza
Inafahamika, msimu huu kutakuwa na ushindani mkali wa namba kutokana na usajili makini uliofanywa na GSM
Hata hivyo Kaseke amesema hilo halimtishi, atahakikisha anaitendea haki heshima aliyopewa kwani haitapendeza yeye kama nahodha kukalia benchi
"Kama mchezaji kiongozi, nitatimiza wajibu wangu ndani na nje ya uwanja. Lakini muhimu nitajituma zaidi ili niwe napata nafasi kwenye kikosi cha kwanza"
"Haitapendeza nahodha kama mimi niwe nakosa namba katika kila mechi, maana nikiruhusu hilo nitakuwa siwapi hamasa wenzangu ya kupambana, raha ya kuwa nahodha upate muda wa kucheza na siyo kukaa benchi," alisema Kaseke
Kaseke alianza majukumu yake vyema kwenye mchezo wa kilele cha wiki ya Mwananchi alipoiongoza Yanga kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir
Akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji upande wa kulia, Kaseke alikuwa na ushirikiano mzuri na beki kinda Kibwana Shomari akimtengea mipira ili 'amwage' maji