Kiungo fundi wa Yanga Haruna Niyonzima anaamini msimu huu hawana sababu ya kutopata mafanikio kutokana na usajili uliofanywa
Niyonzima aliyerejea Yanga mwezi Januari mwaka huu, ameeleza kuvutiwa na uwezo unao-onyeshwa na wachezaji wapya waliosajiliwa na mabingwa hao wa kihistoria
Yanga imesajili nyota wapya 14 ambapo miongoni mwao nyota watano ni raia wa kigeni
Wachezaji hao ni washambuliaji Yacouba Soghne, Michael Sarpong, viungo Mukoko Tonombe, Carlinhos na winga Tuisila Kisinda
"Msimu uliopita tulikuwa na changamoto nyingi hasa eneo la ushambuliaji, lakini msimu huu nadhani kutakuwa na mambo mazuri. Ujio wa washambuliaji wapya umeimarisha eneo hilo pamoja na usajili uliofanywa katika maeneo mengine"
"Tumeanza kucheza pamoja karibuni, lakini matumaini ni makubwa, timu ikishakuwa imeunganika vizuri, tutakuwa na kikosi chenye ushindani mkubwa," alisema Niyonzima
Yanga ilianza msimu kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo ambao mabingwa hao wa kihistoria walitawala
Jumapili wanashuka tena katika dimba la Mkapa kuumana na Mbeya City katika mchezo ambao Wanayanga wanahitaji ushindi