Kikosi cha mabingwa wa kihistoria Tanzania, Yanga leo kinatupa karata yake ya pili ligi kuu ya Vodacom wakishuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Mbeya City katika mchezo utakaopigwa kuanzia saa moja usiku
Huu ni mchezo ambao Yanga haihitaji matokeo mengine zaidi ya ushindi hasa baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Tanzania Prisons
Kwa wiki nzima, Yanga ilijichimbia huko Kigamboni wakifanya maandalizi kuelekea mchezo wa leo
Kwa mara ya kwanza, Yanga itashuka uwanja wa Mkapa wakiwa ndani ya uzi wao mpya waliouzindua karibuni
Ubora wa jezi hizo, umewaongezea hamasa wachezaji na hata mashabiki ambao wanaamini leo Mbeya City hawatachomoka pale kwa Mkapa
Kocha Mkuu wa Yanga Zlatko Krmpotic amedokeza kuwa kikosi chake leo kitakuwa na mabadiliko ukilinganisha kikosi alichotumia mchezo dhidi ya Tanzania Prisons
Baadhi ya wachezaji wa kigeni waliokosekana katika kikosi cha kwanza cha mchezo ule wanaweza kuanza leo
Afisa Mhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz amewataka mashabiki wa timu hiyo wajitokeze kwa wingi uwanja wa Mkapa kuwapa hamasa wachezaji wao ambao siku ya leo wameahidi kuwapa furaha
