Pamoja na kuwa Yanga imeuanza msimu taratibu, jambo moja kubwa kwa mashabiki, wanapaswa kuwa kitu kimoja kuhakikisha hawatolewi kwenye reli
Baada ya mchezo dhidi ya Kagera Sugar, kumejitokeza makundi ya wanaojiita mashabiki wa Yanga ambao wanaonyesha kutomuunga mkono kocha Zlatko Krmpotic
Katika vyombo vya habari mjadala umekuwa mkubwa zaidi, kama mashabiki hawatakuwa makini jambo hili linaweza kuwavuruga
Kwanza, ifahamike Zlatko hana hata mwezi mmoja tangu atue Yanga, anahitaji muda kutengeneza kikosi chake
Lakini pia kwa sasa pamoja na kuwa timu yake haijakaa sawa, anapaswa kuhakikisha timu hapotezi mechi na muhimu zaidi hatoki kwenye reli ya kuwania ubingwa
Presha hii pengine ndio inayomfanya wakati mwingine atumie mbinu ambazo haziwafurahishi mashabiki lakini lengo likiwa kushinda
Zlatko anafahamu kama timu yake haitapata matokeo katika mechi kadhaa, anaweza kutimuliwa licha kuwa sababu za kutofanya vizuri zinaweza kuwepo
Kutimua makocha mwanzoni mwa msimu pia haitakuwa jambo zuri kwa Yanga kwani hata akija kocha mwingine nae atahitaji muda, huo utakuwa mwanzo wa kuvuruga malengo ya msimu
Zlatko ni kocha mzuri, CV yake inajieleza, huwezi kuwa na shaka na kocha ambaye amewahi kufanya kazi na miamba wa soka barani Afrika TP Mazembe na timu kama ZESCO United
Ni bahati mbaya kwake alichelewa kujiunga na Yanga, hakuwa na pre-season na hawezi kufanya majaribio katika mechi
Muunganiko wa timu hautapatikana kwa siku moja, lakini kadiri wachezaji wanavyoendelea kucheza pamoja, utapatikana
Hakuna mwenye shaka juu ya uwezo wa wachezaji waliosajiliwa, ni suala la muda tu Wanayanga watapata furaha ya kweli