Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said amesema ujio wa kocha Cedric Kaze umezingatia malengo waliyoweka ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu na sio kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba tu
Hersi amesema mtaalamu huyo analetwa kwa ajili ya kutengeneza kikosi imara kitakachorejesha heshima ya Yanga hapa nchini pamoja na Kimataifa

"Tunapenda ifahamike kuwa hatumleti Kaze kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba tu, tuna mechi zaidi ya 33 kwenye ligi. Nia yetu ni kutengeneza timu imara yenye ushindani," Injinia Hersi aliiambia Magic FM
Aidha Hersi amesema ujio wa mtaalamu huyo aliyefanya kazi nje ya Afrika katika nchi za Hispania, Ujerumani na Canada, utawanufaisha wachezaji katika Mawasiliano kwani Kaze anazungumza lugha zaidi ya nne
"Kaze anazungumza lugha zaidi ya nne Kihispaniola, Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa hivyo itawawia rahisi wachezaji wetu wanaozungumza lugha moja tu kuwasiliana nae katika kutimiza majukumu yao"
Uongozi wa Yanga unatarajiwa kumtangaza Kaze, raia wa Burundi kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akichukua nafasi iliyoachwa na Zlatko Krmpotic