Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia mabingwa hao wa kihistoria
Kaze amesaini mkataba huo mapema leo mbele ya Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya klabu hiyo
Hafla hiyo ilienda sambamba na utambulisho wa kocha huyo raia wa Burundi
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Simon Patrick ambaye pia ndio Mwanasheria Mkuu wa klabu, amesema, mkataba huo una kipengele cha kuuhuisha pale utakapomalizika
Aidha, Simon amesema mkataba huo umeanza rasmi leo lakini Kaze ataanza majukumu yake rasmi baada ya zoezi la kumkatia vibali kukamilika
Amesema tayari wameanza kufuatilia vibali vya kocha huyo leo hii



Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Msolla amemkaribisha Kaze akimuahidi ushirikiano kutoka kwa uongozi na mashabiki wa Yanga
"Karibu sana Tanzania, kila mmoja wetu ana imani nawe. Kama uongozi tutakupa ushirikiano wote ili kuhakikisha unatimiza majukumu yako vyema," alisema Dk Msolla
"Pia nawaambia mashabiki wetu, ni vyema tukashirikiana na kocha wetu ili aweze kujenga timu imara. Halitakuwa jambo jema kuanza kumpa presha mapema wakati sote tunafahamu, ujio wake ni kwa ajili ya kuimarisha timu kuhakikisha tunaweza kufikia malengo yetu"
Mwenyewe akizungumza kati hafla hiyo, Kaze amesema ujio wake Yanga ni kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo kushnda mataji
Amesema amechelewa kutua nchini kwa sababu alikuwa akifanya tathmini ya kina ya timu yake pamoja na ligi kwa ujumla ili kuhakikisha anafanikisha kazi iliyomleta
Amesisitiza kuwapa furaha mashabiki kwa kandanda safi ikiwa ni pamoja na kutimiza malengo ya kuwania ubingwa wa ligi kuu