Kocha Cedric Kaze ameanza vyema maisha yake ndani ya klabu ya Yanga akifanikiwa kuondoka na alama zote sita katika michezo miwili aliowaongoza mabingwa hao wa kihistoria
Lakini jambo muhimu hapa, pamoja na muda mchache aliokaa na timu, tayari mwanga unaonekana kuwa wapinzani wake watakuwa na kazi ya ziada kuondoka na alama tatu mbele ya kikosi chake pale mambo yatakapokuwa yameiva sawasawa
Kaze alijipa muda wa kuisoma ligi, akipata nafasi ya kuifanyia tathmini kila timu inayoshiriki VPL msimu huu
Kimbinu, Kaze ni kocha aliyekamilika, na wengi watashangazwa na jinsi atakavyokuwa akiwatumia wachezaji wake kulingana na mechi
Kwa aina ya mfumo anaofundisha, wengi walidhani timu yake itakuwa na wakati mgumu mechi za viwanja vya mikoani
Lakini ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC uwanja wa CCM Kirumba, umedhihirisha kuwa hata huko mikoani timu zijipange kwelikweli kucheza na Yanga
Katika mchezo huo, Yanga ilitumia washambuliaji wawili, Kaze alifichua ilikuwa mbinu aliyoamua kutumia baada ya kuwasoma KMC pamoja na mazingira ya uwanja wa CCM Kirumba
Bila shaka keshokutwa Jumamosi, atawapa sapraizi Biashara United kwa kuingia na mbinu nyingine pale Yanga itakapokuwa ikisaka alama nyingine tatu uwanja wa Karume
Kaze amepata muda wa kutosha kukiandaa kikosi chake kuelekea mchezo huo. Yanga imejichimbia jijini Mwanza kwa takribani siku nne kujiandaa na mchezo huo