Mpaka sasa klabu ya Simba imeathirika zaidi na usajili wa aliyekuwa winga wa Yanga Bernard Morrison ambaye usajili wake bado una utata Yanga ikipeleka malalamiko Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi wa michezo (CAS) ikipinga TFF kumhalalisha mchezaji huyo kuitumikia Simba
Kisasi walicholipa Yanga baada ya Simba kumtambulisha mchezaji huyo sio kidogo, kwani mabosi wa GSM 'wakasepa mazima' na aliyekuwa Mtendaji wa klabu ya Simba Senzo Mazingisa ambaye kwa sasa ni sehemu ya wataalam wanaosuka mpango mkakati wa Yanga mpya
Simba bado 'wanaweweseka' na kuondoka kwa Senzo. Taarifa zilizosambaa jana klabu hiyo iliwafuta kazi Meneja wa timu, Kocha wa makipa na Mwanahabari aliyekuwa akisimamia mitandao ya kijamii kwa kile kilichoelezwa kuwa na ukaribu na Senzo
Kuna wakati hata Mwekezaji wa Simba Mohammed Dewji 'Mo' alilalamika kuwa Senzo ameondoka Simba na nyaraka zao muhimu ikiwemo taarifa za mikataba ya wachezaji
Hili ndilo linalowatia presha zaidi kwani wanafahamu jambo lolote linaweza kutokea kwa nyota wao muhimu akiwemo Mzambia Clatous Chama ambaye siku za karibuni amekuwa akiwasumbua sana
Usajili wa Morrison pia umewagharimu zaidi Simba kwani mpaka sasa Mghana huyo hajaonyesha maajabu yoyote kunako klabu hiyo ukilinganisha na wakati alipokuwa kwa Wananchi
Wakati sakata lake na Yanga likiwa bado halijapoa, Morrison anasubiri adhabu ya kufungiwa baada ya kumpiga ngumi mlinzi wa Ruvu Shooting Juma Nyosso kwenye mchezo wa ligi kuu mapema wiki hii ambao Simba ilifungwa bao 1-0