Kesho Jumamosi mchezo wa kwanza wa watani wa jadi msimu huu utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 jioni
Awali mchezo huo ulipangwa kupigwa Oktoba 18 lakini ukapigwa kalenda, hatimaye Novemba 07 imewadia
Yanga inayonolewa na kocha Cedric Kaze, ndio itakayokuwa mwenyeji wa mchezo huo unaovuta hisia za mashabiki wa soka nchini na hata ukanda wa Afrika Mashariki
Kwa mara ya kwanza katika misimu mitatu, mabingwa hao wa kihistoria wataingia katika mchezo huo wakiwa na kikosi kilichokamilika
Kwa misimu ya karibuni, Yanga iliingia katika mechi dhidi ya Simba ikiwa 'underdog' lakini sio kwenye mchezo wa kesho
Kikosi cha Cedric Kaze kina kila sababu ya kuibuka na ushindi, ndio! angalia takwimu, wako bora zaidi kitimu kuliko watani zao Simba
Wakati Simba ikiwa imepoteza mechi mbili, Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote msimu huu
Katika mechi tisa walizocheza, wameshinda saba na kutoka sare mechi mbili
Lakini tunazungumzia timu yenye safu bora zaidi ya ulinzi pia, ukuta wao umeruhusu mabao mawili tu
Yanga inacheza kitimu zaidi, ushindi katika mechi walizoshinda ulitokana na upambanaji wa timu nzima
Hali ni tofauti na watani zao Simba ambao wanamtegemea zaidi kiungo Clatous Chama
Kama nyota huyo kutoka nchini Zambia atawekewa mkakati kabambe wa ulinzi, ni wazi mambo yanaweza kuwaendea 'kombo' Simba
Kwa kocha Kaze, huu ni mchezo wa kumtambulisha rasmi katika ardhi ya Tanzania
Mrundi huyo anafahamu madhara ya matokeo ya mchezo huu kwake, yanaweza kumpaisha au kumshusha chini
Kimbinu, Kaze ni kocha aliyekamilika, hatakuwa tayari kuona timu yake ikipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya watani zao
Na ndio maana aliamua kuwapumzisha baadhi ya wachezaji kwenye mchezo uliopita dhidi ya Gwambina Fc ili kuhakikisha kesho anakuwa na kikosi chake kilichokamilika