Shabiki Mhamasishaji na Mwanachama maarufu wa klabu ya Yanga Jimmy Msindo 'Kindoki' amesema bado wanaamini kiungo Clatous Chama atajiunga na Yanga kwa ajili ya msimu ujao, wakimuandalia zawadi ya gari (Subaru)
Mapema jana Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi klabu ya Simba Mohammed Dewji alitangaza kuwa wamemuongezea mkataba Chama mpaka mwaka 2022
Kindoki amesema wao wanachofahamu kuhusu Chama ni kuwa kila kitu kilishakamilika na muda ukifika mambo yatawekwa hadharani
"Tunafahamu Simba walimnyan'ganya Chama gari baada ya kubaini hataki kuendelea kucheza katika timu yao. Sasa sisi mashabiki, mmoja wetu ametoa zawadi ya gari (Subaru) ambayo akifika nchini tutamkabidhi"
"Hii ni gari nyingine kabisa sio ile tuliyoahidi katika mchezo dhidi ya Simba. Tumeona sio sawa kwa Chama kupata shida wakati tunafahamu msimu ujao tutakuwa nae," alitamba Kindoki
Kwa muda mrefu Chama amehusishwa na klabu ya Yanga. Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Injinia Hersi Said katika moja ya mahojiano yake alisema hawajafanya mchakato wowote wa kutaka kumsajili Chama kwa kuwa wanafahamu ana mkataba halali na Simba lakini alisisitiza kuwa kama wakimuhitaji hawawezi kumkosa