Kuelekea dirisha dogo la usajili ambalo litafunguliwa Disemba 15, tetesi za usajili kuelekea dirisha hilo zimeanza kushika kasi
Yanga wakiwa na hesabu za kutwaa ubingwa msimu huu, tayari wameshasajili mchezaji mmoja, kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza raia wa Burundi
Hata hivyo, inaelezwa mabingwa hao wa kihistoria wanaweza kuongeza mchezaji mwengine katika kuimarisha safu yake ya ushambuliaji
Kinara wa mabao ligi ya Vodacom msimu huu Adam Adam, anatajwa kuingia katika rada za Wananchi
Adam yuko katika kiwango bora sana akiwa na JKT Tanzania, ndiye mchezaji wa kwanza kufunga hat-trik msimu huu
Anaongoza mbio za kuwania kiatu cha dhahabu akiwa ameweka kambani mabao sita kama ilivyo kwa Prince Dube wa Azam Fc
Kwa mara ya kwanza, Adam alijumuishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ambacho juzi kililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia
Huyu ni mchezaji asiyekuwa na mambo mengi sana awapo uwanjani lakini ana jicho kali la kuziona nyavu