Kabla ya mchezo kati ya Azam Fc dhidi ya Yanga, wachambuzi wengi walikuwa hawaipi Yanga nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo wakiamini Azam Fc ndio waliokuwa bora zaidi
Lakini kilichotokea ni tofauti, Yanga ndio iliyokuwa bora zaidi, wakiwapa Azam Fc wakati mgumu kucheza katika uwanja wao wa nyumbani
Pongezi anastahili kocha Cedric Kaze ambaye mbinu zake ziliweza kuinufaisha Yanga ambayo ilipata ushindi wa bao 1-0 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi
Kaze amebainisha kuwa aliwasoma Azam Fc na kubaini ubora na udhaifu wao, hivyoΒ kuja na mpango wa mchezo ambao ulikuwa chachu ya wao kuondoka na alama zote tatu
"Nilipata muda wa kuwasoma Azam Fc, nikabaini udhaifu flani katika kutekeleza mipango yao. Mipango yao huwa inaanzia kwa walinzi wao, hivyo nikachagua wachezaji ambao kazi yao ilikuwa kuhakikisha wachezaji wao hawapandi hivyo kutupa nafasi ya kuwa imara eneo la kiungo"
"Nawapongeza vijana wangu walicheza kwa nidhamu ya hali ya juu, tulikuwa bora kwa muda wote wa mchezo. Ni matokeo ambayo ulistahili kuyapata," alisema Kaze
Aidha Kaze amemsifu mshambuliaji raia wa Burkina Faso Yacouba Sogne kuwa ameanza kurejea katika ubora wake
"Yacouba ameonyesha kiwango kizuri, na ni mchezaji mzuri, kipindi anajiunga Yanga alikua hajacheza kwa takribani miezi mitano kutokana na Corona.Lakini kwasasa anajituma na kufanya vizuri mazoezini, fitness yake ipo vizuri na mimi ndio kocha nataka mchezaji anaejituma ili kupata alama tatu"
Yacouba ndiye aliyetoa pasi iliyozaa bao la Yanga lililofungwa na Deus Kaseke kwenye dakika ya 48
Baada ya mchezo huo, mchezo unaofuata ni dhidi ya JKT Tanzania, utapigwa Jumamosi uwanja wa Benjamin Mkapa