Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said amesema wameridhishwa na mwenendo wa timu baada ya kukamilisha duru ya kwanza ligi kuu ya Vodacom bila ya kupoteza mchezo
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Ihefu Fc jana, Hersi aliwasifu wachezaji wa Yanga pamoja na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Cedric Kaze kwa kuweza kufikia mafanikio hayo katika nusu ya kwanza ya msimu
"Tuliweka wazi malengo yetu ya msimu huu kuwa ni kushinda ubingwa. Mpaka sasa tumekamilisha mzunguuko wa kwanza tuko kileleni mwa msimamo wa ligi na hatujapoteza mchezo. Hili ni jambo la kupongeza wachezaji, benchi la ufundi, viongozi pamoja na mashabiki wetu kwani kila mmoja kwa nafasi yake ameonyesha uwajibikaji mkubwa"
"Timu yetu imeendelea kuimarika siku hadi siku, bado hatujamaliza kazi lakini ni faraja kwenda mapumziko baada ya mzunguuko wa kwanza tukiwa tunaongoza," alisema Hersi
Aidha Hersi amedokeza kuwa wako mbioni kukamilisha usajili wa mchezaji mmoja mkubwa ambaye ujio wake utatikisa nchi!
"Tulishasema, utaratibu wetu wa usajili ni huu, mchezaji yeyote tunayemsajili sasa lazima awe mchezaji wa kikosi cha kwanza, hivyo niwahakikishie kipindi hiki tutafanya usajili mmoja ambao ni mkubwa sana kama wa Saido , ni usajili ambao ni mkubwa sana na bora sana ndani ya Yanga sc na isitoshe kwa kipindi cha dirisha dogo la usajili ni lazima ulete mtu bora wakuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza," alisema Hersi