Ditram Nchimbi amekuwa mchezaji muhimu sana kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kinachonolewa na kocha Etienne Ndayiragije
Tangu Ndayiragie akabidhiwe mikoba ya kuinoa Stars, hakuwahi kumuacha nje ya kikosi chake Nchimbi,maarufu 'Duma' na kwa hakika hajamuangusha
Hata ushiriki wa Tanzania kwenye fainali za michuano ya CHAN 2020 zinazoendelea huko Cameroon, Nchimbi amehusika kuanzia hatua ya awali kabisa
Bao lake la dakika ya 80 kule Sudan liliihakikishia Tanzania kutinga fainali za michuano hiyo kwa mara ya pili baada ya ushindi wa mabao 2-1 ugenini
Aidha ushindi uliopatikana kule Cameroon kwenye mchezo dhidi ya Namibia, pasi yake mahiri ya kichwa iliwekwa kambani na Farid Mussa nyota wanayecheza nae Yanga
Ndayiragije amemtumia Nchimbi kama mshambuliaji wa kati kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukaba pale mbele na kasi yake ni silaha muhimu anapotokea pembeni huku krosi zake zikiwa na faida kubwa
Mwamba huyu ni sehemu ya kikosi cha kocha wa Yanga Cedric Kaze ambaye bila shaka atakuwa akifuatilia michuano ya CHAN 2020 akiwa na tabasamu kwani nyota wake walio katika kikosi cha Stars wanafanya vizuri
Kaze anafahamu michuano hiii inawaimarisha wachezaji wake na kuwaongezea kujiamini wale ambao walikuwa wakisuasua katika kikosi chake
Farid Mussa, Deus Kaseke na Nchimbi ni wachezaji ambao wananufaika sana na michuano hii wakati kwa Bakari Nondo Mwamnyeto na Feisal Salum 'Fei Toto' michuano hii inazidi kuwakomaza