Mshambuliaji wa zamani wa Yanga Amisi Tambwe amethibitisha kuwa klabu hiyo imezuiwa kufanya usajili kwa madirisha matatu hadi pale itakapomlipa madai anayowadai mabingwa hao wa kihistoria
Tambwe aliyeachwa na Yanga mwaka 2019 alikuwa akiidai klabu hiyo fedha za nyuma za usajili na malimbikizo ya mishahara yanayofikia Tsh Milioni 44
Mkali huyo wa kuzifumania nyavu, alipeleka malalamiko yake FIFA baada ya kutokea mvutano baina yake na uongozi wa Yanga kuhusu kiasi cha fedha alizokuwa akidai
Yanga pia ilipeleka malalamiko FIFA ikipinga madai hayo ya Tambwe lakini usiku wa kuamkia leo Tambwe na Wakala wake wamethibitisha kuwa Yanga imeamuriwa kumlipa Tambwe kiasi cha Tsh Milioni 44
Na sasa wamezuiwa kufanya usajili kwa madirisha matatu mpaka pale watakapomlipa fedha zake zote
"Nimetaarifiwa na Wakala wangu usiku huu (jana) kuwa Yanga imefungiwa kusajili kwa madirisha matatu mpaka pale watakaponilipa fedha ninazodai"
"Kulikuwa na madai nimefungua FIFA kuitaka Yanga inilipe fedha zangu. Wao walifungua kesi CAS wakipinga madai hayo lakini sasa nimeshinda na usiku huu nimetaarifiwa Yanga wameamuliwa kunilipa na hawatasajili mpaka watakapolipa deni," alisema Tambwe
Aidha imeelezwa kuwa pamoja na kuzuiwa kusajili, kama Yanga hawatalipa deni hilo mpaka muda ukamalizika, wanaweza kukumbana na adhabu zaidi ikiwa ni pamoja na kulipa na faini au kukatwa alama
Misimu mitatu nyuma Yanga ilikumbwa na hali ngumu ya kiuchumi iliyopelekea kulimbikiza madeni mengi
Sio Tambwe tu anayeidai Yanga, upo msululu wa wachezaji na makocha waliopita Yanga kati ya mwaka 2016 na 2019
Ni hivi karibuni tu wamemalizana na Mwinyi Zahera aliyelipwa fedha zake zaidi Tsh Milioni 100 alizokuwa akidai
Zahera naye alipeleka malalamiko FIFA
Uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla umeeleza kuwa wakati wanaingia madarakani walikuta rundo la madeni, wamekuwa wakilipa madeni hayo taratibu