Kama hakutakuwa na mabadiliko ya Ratiba, mchezo wa pili wa watani wa jadi kati ya Simba dhidi ya Yanga unapaswa kupigwa Februari 20, Simba wakiwa wenyeji wa mchezo huo
Huo utakuwa mtanange wa pili baina ya timu hizo kwenye ligi lakini utakuwa mtanange wa tatu kuzikutanisha timu hizo msimu huu
Watani hao wa jadi walikutana kwenye mchezo wa fainali michuano ya kombe la Mapinduzi, Yanga wakiibuka washindi na 'kusepa' na taji hilo
Baada ya kuwakosa kosa katika mchezo wa duru ya kwanza, hesabu za kocha Cedric Kaze itakuwa kuondoka na alama zote tatu katika mchezo huo ili kujiongezea kasi katika mbio za ubingwa
Aidha maboresho ya kikosi yaliyofanywa katika usajili wa dirisha dogo, yanampa Kaze kiburi kuelekea mchezo huo huku mashabiki wa Yanga wakicheeka!
Saido Ntibazonkiza, Fiston Abdul Razak na Tuisila Kisinda hawa watakuwa na kazi maalum kwenye lango la Simba
Kwa jinsi safu ya ulinzi ya Simba inavyocheza, huoni ni kwa namna gani wataweza kuwadhibiti washambuliaji hawa
Ntibazonkiza tayari amedhihirisha makali yake, Kisinda tayari wanamfahamu wakati Fiston ndio kwanza ametua lakini moto wake haupimiki!
Huu ni mchezo ambao safu za ulinzi za timu zote zitakuwa katika majaribu makubwa lakini ukiweka mzani, utaona safu ya Yanga iko imara zaidi ukilinganisha na watani zao
Uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga ulidhihiri hata kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi ambapo waliweza kuwadhibiti washambuliaji wa Simba ambao katika mchezo huo hawakupiga hata shuti moja lililolenga lango!
Kwa hakika ni mchezo ambao Yanga wanapaswa kushinda, ni matokeo ambayo yatawaongezea morali katika mbio za ubingwa msimu huu