Jana ilikuwa siku mbaya sana kwa mashabiki wa Yanga ambao waliishuhudia timu yao ikilazimishwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam
Wengi hawakufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yao hasa kwenye kipindi cha kwanza, Kagera Sugar wakifunga mabao yao yote katika kipindi hicho
Lakini pia suala la waamuzi nalo likaibuka, Wanayanga wanaona hawakutendewa haki na Mwamuzi wa mchezo huo
Baada ya mchezo kumalizika, mashabiki walimvaa Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla aliyekuwepo uwanjani hapo
Wengi walilalamika kwa uongozi wake kukaa kimya wakati timu haitendewi haki katika baadhi ya michezo
Huo ni mchezo wa pili mfululizo mashabiki wanapaza sauti zao kutokana na matukio ya kuonewa hasa kunyimwa mikwaju ya penati
Yanga imekuwa ikipigwa faini karibu kila mchezo kwa makosa yanayofanywa na mashabiki wake. Sehemu ya makosa hayo waamuzi wanachangia kwa kuamsha hisia za mashabiki
Mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City nashabiki walimrushia chupa za maji mwamuzi wa mchezo na hata jana baada ya mchezo dhidi ya Kagera Sugar
Unaweza kusema tayari faini nyingine inainyemelea Yanga kutokana na matukio ya mashabiki katika mchezo wa jana
Kuna ulazima kwa uongozi wa Yanga kuibana Bodi ya Ligi kushughulikia changamoto hizi za waamuzi ambazo zinaonekana kushamiri zaidi katika mechi za hivi karibuni walizocheza Yanga
Kama hili halitafanyika, ni wazi huko mbeleni mashabiki wanaweza kufanya matukio ya hatari zaidi ambayo yanaweza kuichafua taswira ya klabu ya Yanga
Ifahamike msimu huu Wanayanga wana matumaini makubwa kwa timu yao kuwa inaweza kushinda ubingwa wa ligi kuu