Kuna baadhi ya mechi uwezo wa mchezaji mmoja mmoja unaweza kuamua matokeo hasa pale mambo yanapokuwa magumu
Nakumbuka mchezo wa kwanza wa ligi ambao kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza alicheza ilikuwa dhidi ya Dodoma Jiji kule mkoani Arusha
Ulikuwa mchezo mgumu sana kwa Yanga iliyoruhusu bao la mapema kabisa
Katika ushindi wa mabao 3-1 Ntibazonkiza alihusika katika mabao mawili, akifunga bao la pili kwa mpira wa adhabu na kutengeneza bao la tatu lililofungwa na Bakari Nondo Mwamnyeto


Ni moja ya michezo ambayo uwezo binafsi wa Ntibazonkiza uliisaidia Yanga kuondoka na ushindi dhidi ya Dodoma jiji waliokuwa wagumu kwelikweii
Ntibazonkiza pia akahusika katika ushindi wa mabao 3-0 ambao Yanga ilipata dhidi ya Ihefu Fc mkoani Mbeya na mchezo uliofuata dhidi ya Tanzania Prisons akafunga bao la kusawazisha na kuinusuru Yanga na kipigo kule Rukwa
Ntibazonkiza yuko nje tangu alipoonekana mechi dhidi ya Prisons na baadae kucheza kwa dharura mechi ya fainali kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba kule visiwani Zanzibar mchezo ambao ulimuongezea madhara ya majeraha aliyokuwa amepata

Kwa hakika Yanga inamuhitaji sana Ntibazonkiza dimbani haraka iwezekanavyo kwani anapokuwa uwanjani wakati wowote anaweza kufanya kitu chenye faida kwa timu
Uongozi wa Yanga umewahakikishia mashabiki kuwa Ntibazonkiza anaweza kurejea uwanjani haraka
Uwepo wa nyota huyu kwenye kikosi utaongeza matumaini katika mbio za kuwania ubingwa