Uongozi wa klabu ya Yanga umewasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) juu ya matukio ya uonevu wanayofanyiwa na waamuzi katika mechi zao za ligi kuu
Kaimu Katibu wa Yanga Haji Mfikirwa amesema wamewasilisha malalamiko mbalimbali kwa TFF kuhusu madai yao mengi tu
"Tumewasilisha malalamiko yetu kwa TFF kuhusu masuala mbalimbali, kesi ya Bernard Morrison, waamuzi na hizi faini tunazopigwa kila wakati"
"Wanatupiga faini sababu ya mashabiki kufanya vurugu, sisi wenyewe tunawaasa mashabiki kutokiuka taratibu za mpira wa miguu lakini wao wanaona waamuzi wanavyoionea timu yao
"Kuna nyakati mashabiki wanatuuliza sisi kwanini tunakaa kimya, tumeamua kuyafikisha kwa umma pengine wenye mamlaka watashtuka waone kitu cha kufanya," amesema Mfikirwa
Uonevu ukizidi tunajitoa VPL
Nae Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema wamechoka kulalamika kwa uonevu wanaofanyiwa na waamuzi
Kesho Yanga ikitarajiwa kucheza mechi ya ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, Mwakalebela amesema kama waamuzi wataendelea kuwaonea, basi hawatasita kuchukua maamuzi magumu
"Sisi Yanga hatutendewi haki na vyombo vinavyosimamia mpira, TFF na Bodi ya ligi, Kamati ya Saa 72, Kamati ya Waamuzi na mamlaka nyingine za soka, ndio maana tumekuwa tukipoteza pointi kwenye mechi nyingi"
'"Tumenyimwa penati dhidi ya Mbeya City, dhidi ya Kagera Sugar na mwisho tunakuwa tunakosa pointi katika hali ya kuonewa mpaka tunajiuliza kuwa, je, kwa mazingira haya kuna bingwa ameandaliwa?"
"Kwenye mchezo wetu wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar hatutarajii kuona matukio ya uonevu wa waamuzi yakiendelea"
"Kama hakutakuwa na haki, kamati ya utendaji itatoa tamko juu ya ushiriki wetu katika ligi kuu Tanzania Bara," amesema