Kama unadhani Wananchi hawako makini katika vita ya kuwania ubingwa, utakuwa unajidanganya kwani mabingwa hao wa kihistoria wana mkakati mzito kuhakikisha wanashinda ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya 28 msimu huu
Hitaji la ubingwa ni la kila mdau wa Yanga kuanzia wadhamini mpaka mashabiki
Zipo ahadi nyingi zimetolewa kwa wachezaji kama watafanikisha hitaji hili la kila Mwanayanga
Miongoni mwa ahadi hizo ipo ya GSM mwenyewe ambaye atatoa donge nono kama ubingwa utaelekea Jangwani
Yanga ilipotwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu, GSM walitoa kitita cha Tsh Sh300 milioni kama motisha kwa wachezaji
Mshauri wa Yanga, Senzo Mazingisa amesema kuwa kitu pekee ambacho wachezaji wanatakiwa kufanya ni kupambana na kutwaa ubingwa kwani bosi wao, Ghalib Mohamed yupo tayari kuwapa zawadi nono.
Senzo alisema wachezaji wanapaswa kutambua kuwa furaha ya Wanayanga na mabosi wao ni kuona ubingwa unatua Jangwani
"Kitu pekee ambacho bosi anatusisitiza ni kuhakikisha timu inachukua ubingwa, sipati picha timu ikichukua ubingwa furaha yake itakuwaje"
"Kama tukichukua ubingwa najua kabisa atatoa zawadi kubwa zaidi ya ile wachezaji walipata kwenye Mapinduzi, anapenda timu ishinde ligi"
"Wachezaji wanataka pesa nyingi kama zawadi, basi wanatakiwa wabebe ubingwa wa ligi na ninaamini hilo linawezekana," Senzo alinukuliwa na Mwanaspoti
Yanga mpaka sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 49 baada ya kucheza mechi 21, huku watani zao, Simba wakicheza mechi 18 wakikusanya pointi 42 wakati Azam FC wanashika nafasi ya tatu katika mechi 20 walizovuna pointi 36.