Baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ken Gold katika mchezo wa raundi ya nne ya michuano ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kutinga hatua ya 16 bora, timu ya Yanga sasa inaelekeza nguvu zake kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union utakaopigwa mkoani Tanga Alhamisi, March 04 2021
Mshauri Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa amesema wanatarajia mchezo wenye upinzani mkali lakini wanapaswa kushinda mchezo huo
"Nawaambia mashabiki wa Yanga hatupaswi kuangalia nini wapinzani wetu Simba wanafanya, muhimu ni kuhakikisha tunaweka mkazo kwenye timu yetu ili tupate matokeo yatakayotusaidia kufikia malengo"
"Mchezo unaofuata ni wa VPL dhidi ya Coastal Union mkoani Tanga. Utakuwa mchezo mgumu lakini tutapambana kuhakikisha tunapata alama zote tatu," alisema Senzo
Baadhi ya mashabiki wameonekana kutofurahia ushindi wa bao 1-0 ambao Yanga walipata dhidi ya Ken Gold wakati watani zao Simba wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon
Hata hivyo msimu huu Yanga imekuwa na mwenendo huo, wakati mwingine ikionekana kushinda kwa taabu baadhi ya mechi zake lakini ndio wako kileleni mwa msimamo wa ligi
Mabingwa hao wa kihistoria, hata waliposhiriki michuano ya kombe la Mapinduzi visiwani Zanzabar, walitinga hatua ya fainali wakiwa wamefunga mabao mawili tu lakini walifanikiwa kuwa mabingwa mbele ya Simba ambao waliinga fainali wakiwa wamefunga mabao saba
Kocha Cedric Kaze amesisitiza jambo muhimu kwake wakati huu ni kuona wanashinda mechi zao bila ya kujali idadi ya mabao wanayofunga sasa kwani anaamini wakati utafika timu yake itafunga mabao mengi