Pamoja na kupoteza mchezo dhidi ya Coastal Union hapo jana, wachezaji wa Yanga itabidi wajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutumia nafasi chache walizotengeneza
Kocha Cedric Kaze atalaumiwa kwani ndiye aliyechagua wachezaji 11 na wale 7 wa akiba kwa ajili ya mchezo huo
Lakini kwa hakika baadhi ya wachezaji wanamwangusha na pengine anapaswa kuchukua uamuzi mgumu kubadili kikosi chake
Farid Mussa ni miongoni mwa wachezaji wanaoaminiwa sana na Kaze, lakini bado hajafanya kile kilichotarajiwa
Farid jana alikosa goli la wazi ambalo kwa mchezaji wa kariba yake alipaswa kufunga
Yanga ilimrejesha Farid kutoka Hispania ambako alicheza kwa takribani misimu minne, kiwango chake hakilingani na mchezaji aliyewahi kucheza nje ya nchi
Alipoingia Kaseke alionyesha tofauti kubwa, huyu ni mchezaji ambaye Kaze anapaswa kumuamini kwa asilimia 100
Kaseke ndiye kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga, unapoona anaanzia benchi hasa katika mechi hizi za mikoani ni jambo la kushangaza kidogo
Katika mchezo wa jana Fiston Abdul Razak alionyesha utofauti kidogo, alihusika katika nafasi mbili muhimu akisababisha mkwaju wa penati ambao Tuisila Kisinda alikosa lakini pia ndiye aliyetoa pasi iliyozaa bao lililofungwa na Kisinda
Pia alitengeneza nafasi nyingine ambayo Kaseke alishindwa kuitumia katika kipindi cha pili
Michael Sarpong nadhani sasa imefika wakati anapaswa kujitathmini. Yawezekana ligi ya Tanzania ameshindwa kuimudu kwani amepewa nafasi kila mara lakini ameshindwa kuonyesha makali
Ni wakati sasa kocha Kaze kumjaribu Waziri Junior sambamba na Fiston ambaye ameonyesha kuwa mzuri katika kutengeneza nafasi
Farouk Shikhalo hatabiriki, ziko nyakati anafanya vizuri sana lakini wakati mwingine anafanya makosa yanayoigharimu timu
Bado anaonekana kuwa na changamoto katika kufanya maamuzi kwenye mipira ya krosi na kufungwa kirahisi mipira ya chini
Bao la kwanza walilofunga Coastal Union lilitokana na makosa aliyofanya na kujikuta yeye na walinzi wake wote wanafuata mpira na walipoukosa ikawa rahisi kwa Msagati kufunga. Hata bao alilofunga Mudathir, alipaswa kuokoa mpira ule
Halitakuwa jambo la kushangaza tukiona Metacha anarejea langoni kwenye mchezo ujao dhidi ya Polisi Tanzania
Haikuwa siku nzuri kwa safu ya ulinzi, Bakari Nondo Mwamnyeto na Lamine Moro walifanya makosa mengi
Mara kadhaa Mwamnyeto alifanya makosa ambayo pengine yalichangiwa na presha ya kucheza Mkwakwani dhidi ya waajiri wake wa zamani
Katika mchezo ule, Mwamnyeto alitarajiwa kucheza kwa utulivu zaidi kwani alikuwa akicheza nyumbani lakini haikuwa hivyo
Hamasa nje ya uwanja muhimu
Wapo waliotoa maoni kuwa Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla anapaswa kufanyia marekebisho Kamati zake za hamasa kwa kuwajumuisha watu wanaolijua soka letu na fitna zake
Suala la uzoefu wa benchi la ufundi nalo limezungumza sana. Kaze anapaswa kufanya kazi na watu wenye uzoefu na ligi kuu ya Tanzania Bara. Ukiangalia idadi ya watu alionao katika benchi lake la ufundi wanakosa uzoefu huo
Ndio maana mashabiki wanapaza sauti kutaka Juma Mwambusi arejeshwe kama amepona maradhi yaliyokuwa yakimsumbua
Mchezo dhidi ya Coastal Union Kaze alikosa mbinu mbadala, kwani alikosa ushauri sahihi juu ya mbinu ambayo alipaswa kuitumia
Matokeo yake tukaishuhudia Yanga iliyokuwa ikibutua tu mpira mbele
Timu haiwezi kushinda bila mipango, hata kama tunacheza katika viwanja vyenye changamoto lazima tuweke mipango ya kusaka ushindi. Kubutua tu mipira mbele ni kuwarahisishia kazi walinzi wa timu pinzani
Coastal Union walikuwa bora zaidi kuliko Yanga kwa sababu wao waliweka mpira chini. Walifanya mipango na wakafanikiwa kufunga mabao yao
Tunawasifu Coastal Union kuwa bora, lakini ni sisi wenyewe tuliojipiga risasi ya mguu