Vinara wa ligi kuu ya Vodacom Yanga leo watakuwa na nafasi ya kusahihisha makosa yao watakapowakabili Polisi Tanzania katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha
Yanga ilifungwa mabao 2-1 katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union, leo wanahitaji ushindi ili kuwatuliza mashabiki wao waliokerwa na kipigo hicho
Lakini pia Wananchi wanahitaji alama zote tatu ili kuhakikisha wanabaki katika mpango wao wa kushinda ubingwa msimu huu, matokeo tofauti na ushindi yataendelea kuirahisishia kazi Simba ambayo itakuwa na faida ya kucheza mechi zake za viporo baadae
Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze huenda akafanya mabadiliko ya kikosi chake leo huku akitarajiwa kuwakosa baadhi ya wachezaji ambao ni majeruhi
Nahodha Lamine Moro na Michael Sarpong walipata majeraha katika mchezo dhidi ya Coastal Union huku mshambuliaji Ditram Nchimbi akirejea kikosini baada ya kukosa mchezo huo
Yanga ilitua Arusha juzi, wakikamilisha maandalizi yao kuelekea mchezo huo jana jioni
Huu ni mchezo ambao Yanga inahitaji ushindi, matumaini ya kila Mwanayanga ni kuona wachezaji wanajituma leo kuhakikisha wanapata matokeo