Klabu ya Simba SC ni miongoni mwa timu zilizowasilisha maombi ya kutumia Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar kwa ajili ya kucheza mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).
Hatua hiyo inakuja kufuatia changamoto ya upatikanaji wa viwanja vinavyokidhi viwango na masharti ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Kwa sasa, Uwanja wa Benjamin Mkapa upo kwenye matengenezo, huku Uwanja wa Uhuru ukihitaji maboresho zaidi ili kukidhi vigezo vinavyotakiwa.
Uongozi wa New Amaan Complex umethibitisha kupokea maombi kutoka kwa klabu zinazohitaji kutumia uwanja huo, huku ukieleza kuwa tayari umefanyiwa maboresho na kufanyiwa tathmini na CAF.
Kwa mujibu wa kanuni za CAF za mwaka 2022, mechi za hatua ya makundi ya mashindano ya klabu barani Afrika zinapaswa kuchezwa katika viwanja vya Daraja la Tatu (Category 3), ambavyo vinatakiwa kukidhi mahitaji mbalimbali ikiwemo usalama, miundombinu bora na mifumo ya matangazo ya televisheni.
Kwa upande wa ushiriki wa timu za Tanzania katika mashindano ya msimu huu, Simba inatarajia kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya saba, huku watani wao wa jadi Yanga SC wakitarajia kushiriki kwa mara ya tano.
Wakati huo huo, Azam FC na Singida Black Stars zinatarajia kuiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup), kila moja ikilenga kufanya vizuri katika mashindano hayo.