Baada ya tamko la SportPesa hapo jana kutoridhishwa na uamuzi wa Yanga kusaini mkataba wa udhamini wa muda mfupi na kampuni ya Haier kwa ajili ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika, Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amesema kuna majadiliano yanaendelea kati yao na SportPesa
Hersi amesema Yanga inaiheshimu SportPesa kuwa ndiye Mdhamini Mkuu wa klabu hiyo, waliwajulisha uamuzi wao wa kuingia makubaliano na Haier wakifahamu CAF hairuhusu udhamini wa kampuni za ubashiri kuanzia hatua ya makundi ya michuano yao
"Tuna majadiliano ya kina na SportPesa ambao ndiyo Wadhamini wetu wakuu. Yanga inafuata na kuheshimu taratibu zote za kimkataba na SportPesa"
"Mazungumzo yetu yalikuwa wazi katika kusaini mkataba na Haier. Hatuwezi kuitumia SportPesa katika michuano ya CAF, hivyo Yanga iliona inaweza kutafuta mdhamini mwingine wa muda"
"Tuna mawasiliano yote wakati tunafanya nao. Lakini si vyema kuweka wazi kila kitu. Taratibu za kiutendaji zinakwenda vyema na tutatapokuwa tumemaliza kila kitu tutakuja kukiweka hadharani," alisema Said
SportPesa imetaka fidia kutoka kwa klabu ya Yanga kwa kuwa wao ndio wana haki ya kukaa kifuani kwenye jezi ya Yanga kwa miaka mitatu 2022-25