Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema kikosi cha Yanga kinaondoka leo jijini Dar es salaam majira ya saa 9 kuelekea Tunisia kupitia Dubai ambako watawasili majira ya saa ya 3:50 usiku
Kesho asubuhi saa 2:40 Yanga itaondoka Dubai kuelekea Tunis tayari kwa mchezo dhidi ya Monastir
Mchezo utapigwa katika dimba la Stade Olympique Hammadi Agrebi Jumapili Februari 12 kwa kuwa uwanja wa Monastir haukukidhi vigezo vya CAF
Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi ndipo Yanga ilishinda dhidi ya Club Africain
Yanga inaondoka na wachezaji 25 akiwemo mlinda lango Aboutwalib Mshery ambaye anakwenda Tunisia kwa ajili ya matibabu
Viongozi tisa wako kwenye msafara huo ambapo Mkuu wa msafara ni Seif Gulamali kwa upande wa Yanga
Kocha Nasreddine Nabi tayari ametangulia Tunisia
Katika hatua nyingine, Kamwe ametangaza viingilio kuelekea mchezo wao wa kwanza wa nyumbani dhidi ya TP Mazembe ambao utapigwa Februari 19 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa
Kamwe amesema dhamira yao ni kuona wanaujaza uwanja wa Benjamin Mkapa na kuhakikisha wanashinda mchezo huo na nyingine mbili zitazofuata ili kufikia malengo ya kutinga robo fainali
"Historia inaonyesha hatukuwa na matokeo mazuri kwenye hatua ya makundi katika miaka ya nyuma lakini msimu huu tuko tayari, tumedhamiria kufanya vizuri na kutinga robo fainali"
"Tunataka mashabiki wetu wawe na utamaduni wa kununua tiketi mapema ndio maana tumetangaza bei za vingilio vya mchezo wetu wa kwanza nyumbani dhidi ya TP Mazembe ambao utapigwa Jumapili, Februari 19"
"VIP A ni Tsh 30,000/-, VIP B ni Tsh 20,000/-, VIP C ni Tsh 10,000/- na Mzunguuko ni Tsh 3,000/- kama utanunua tiketi yako sasa na Tsh 5,000/- kama utanunua tiketi siku ya mchezo"
"Tunajua umuhimu wa alama tisa katika mechi za nyumbani hivyo tunaanza na TP Mazembe, ni lazima tuhakikishe alama zote tatu zinabaki," alisema Kamwe