Madaktari wa Yanga wameokoa uhai wa abiria mmoja wakati kikosi hicho kikiwa safarini kwenda nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir utakaochezwa Jumapili ya Februari, 12
Kwa mujibu wa kituo cha redio cha UFM wakati timu hiyo ikiwa safarini rubani wa ndege la Shirika la Emirates alisikika kupitia vipaza sauti akisema;
"Tunaomba kama kuna daktari yoyote apite mbele, tuna mgonjwa yupo kwenye hali ya hatari."
Jitihada za madaktari wa Yanga za kuokoa maisha ya abiria huyo zilizaa matunda baada ya kupatiwa matibabu na kurejea kwenye hali yake ya kawaida jambo ambalo liliifanya ndege hiyo kuendelea na safari na kutua jiji la Tunis kwa wakati uliotakiwa.
Kwa mujibu wa Daktari wa Yanga, Moses Etutu alinukuliwa akisema abiria huyo alikuwa na changamoto ya sukari pamoja na mambo mengine.
Aidha kwa taarifa iliyotolewa na wahudumu wa ndege ilikuwa inahitaji kutua uwanja wa karibu ili kuokoa maisha ya abiria huyo ingawa jitihada za madaktari wa Yanga ziliwafanya kusitisha mpango huo na kuendelea na safari kama ilivyopangwa.