Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda, amesema tayari wamefanikiwa kuona ubora wa Horoya AC ulipo na udhaifu wao, hivyo wataenda nchini Guinea kikamilifu kwa ajili ya kusaka pointi muhimu katika mchezo huo wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika
Simba inatarajiwa kuondoka nchini Alfajiri ya Alhamisi kuelekea Guinea tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumamosi, Februari 11
Mgunda amesema wanafahamu wanaenda kucheza na aina gani ya timu na wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kusaka matokeo chanya.
Amesema wanahitaji kupata matokeo mazuri, hivyo wamewaelekeza wachezaji wao kuwa makini kwa kutumia vizuri nafasi wanazotengeneza kupata bao na kutoruhusu Horoya AC kufanya mashambulizi lango mwao.
"Tumeona ubora wa Horoya AC, wako vizuri, tunaenda kwa tahadhari kubwa, wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo huo ni kutafuta pointi, tunaendelea kuimarisha kikosi hususan safu ya ulinzi kuwa makini na washambuliaji wa timu pinzani"
"Wakati tukipambana wapinzani wasipate bao, tunahitaji kuwa makini kutafuta alama hata moja katika mchezo huo wa ugenini kabla ya kurejea nyumbani kwa ajili ya kutafuta pointi tatu za nyumbani," alisema Mgunda



