Wakiwa katika uwanja wao wa Emirates, Arsenal wameshindwa kutamba mbele ya Manchester City wakikubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Premia
Ni matokeo ambayo sio tu kuwa yanawatia hofu mashabiki wa Arsenal waliojaa matumaini kuwa msimu huu wanaweza kuwa mabingwa baada ya kusubiri kwa miaka 19, bali pia yamewaonyesha Mikel Arteta ana kazi ya kufanya ili kutimiza ndoto hiyo
Ulikuwa mchezo ambao Arsenal walitawala kwa muda mwingi lakini City wakatumia nafasi muhimu walizopata kupata ushindi
Kelvin De Bruyne alitumia makosa ya mlinzi Takehiro Tomiyasu kurudisha mpira mfupi kwa kipa kuiandikia City bao la kuongoza kwenye dakika ya 24
Arsenal wakakomboa bao hilo kupitia mkwaju wa penati kwenye dakika ya 42 baada ya Nketiah kufanyiwa madhambi na mlinda lango wa City Ederson
Manchester City walikuwa bora zaidi kwenye kipindi cha pili na kufanikiwa kuongeza mabao mengine mawili kupitia kwa Glealish na Haaland aliyefunga bao lake la 26 msimu huu
Man City imepanda kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya mabao dhidi ya Arsenal huku timu zote zikiwa na alama 51
Arsenal wana mechi moja ya kiporo dhidi ya Aston Villa ambapo kama watashinda basi watarejea tena katika nafasi yao
Hofu ya mashabiki wa Arsenal ni mwenendo wa timu yao kwani katika mechi tatu zilizopita wameambulia alama 1 tu