Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Ahmed Ally amewataka mashabiki watumie vyema siku ya leo kuweka tiketi zao mikononi tayari kwa mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Raja Casablanca ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Ahmed amesema Simba haijawahi kuwa na hofu katika mechi kubwa, Wanasimba wanapaswa kuujaza uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya kesho ili kuwaongezea hamasa wachezaji wao katika mchezo ambao Simba inahitaji ushindi
Ahmed jana alifanya hamasa katikati ya jiji la Dar es salaam akianzia Msimbazi na baadae kumalizia Soko la Karume
Akiwa na 'kispika' chake, Ahmed aliwahakikishia mashabiki wa Simba kuwa kesho hakutakuwa na matokeo mengine zaidi ya ushindi kwa Simba
"Hakuna cha mpira unadunda, hakuna cha matokeo matatu. Tokeo ni moja tu (ushindi). Ndugu zangu wa Karume nimekuja kuwaalika, hili tunalopanga kulifanya halitafanikiwa kama hamtakuwepo uwanjani," alisema Ahmed
Leo ndio siku ya mwisho ya maandalizi kuelekea mchezo huo utakaopigwa kesho saa 1 usiku
