Timu ya KMC imejikuta katika wakati mgumu kutokana na kuwa na mechi ngumu mfululizo dhidi ya Yanga na Azam huku ikiwa katika nafasi ya 12 ya msimamo wa Ligi Kuu Bara
KMC ambayo ipo nafasi ya 12 ikiwa na alama 23, Jumatano inatarajia kuvaana na Yanga huku Jumamosi wiki hii ikishuka dimbani dhidi ya Azam FC ambayo na yenyewe inawania angalau kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Afisa Habari wa KMC, Christina Mwagala, amesema kipindi walichonacho kwa sasa ni kigumu kutokana na kukabiliwa na michezo migumu dhidi ya Yanga na Azam zote zikiwa zinawania nafasi za juu.
"Mechi yetu na Yanga itakuwa ngumu kwa kuwa wao wapo katika presha ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa, pia wanaongoza kwenye msimamo, hivyo wanahitaji kupata matokeo mazuri"
"Pia ukiangalia wamepishana pointi sita na wapinzani wao, Simba hivyo, watahitaji ushindi ili wasipoteze pointi kwa kupata alama tatu," alisema na kuongeza:
"Ukiangalia katika kipindi hiki, KMC inapitia wakati mgumu zaidi ya vipindi vyote kwani Jumatano tunacheza na Yanga kisha Jumamosi tunacheza na Azam ambayo inahitaji kujiweka vizuri, mechi zote ngumu huku tukiwa nafasi ya 12"
"Ukiachana na michezo hiyo wanaotufuatia nyuma wanapambana ili na wao waweze kuja juu, lakini tumejipanga kufanya vizuri na hali ya kikosi ipo vizuri wachezaji wetu ambao walikuwa majeruhi wamerejea kwa ajili ya kupambana ili kumaliza katika nafasi nzuri," alisema Mwagala.
Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama 59, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 53, zote zikiwa zimecheza mechi 22, huku Singida Big Stars iliyopo nafasi ya tatu yenyewe na alama 44 ilizozipata kwa kushuka dimbani mara 23.
Azam FC iliyoshuka dimbani mara 22, yenyewe ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 43, jambo ambalo linaongeza ushindani kati yao na Singida Big Stars kuwania kumaliza nafasi ya tatu