Wakiendelea kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ihefu utakaopigwa Ijumaa ya wiki hii, timu ya Dodoma Jiji imekiri mambo ni mazito kwenye ligi kwa sasa wakati ikielekea ukingoni
Dodoma inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa timu 16 ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi 23, ikishinda saba, sare tatu na kupoteza 13, huku ikifunga mabao 17 na yenyewe kufungwa 29.
Katika mechi saba ilizosalia nazo nne zitakuwa za nyumbani dhidi ya Ihefu, Polisi Tanzania, Coastal Union na KMC, huku tatu za ugenini kuvaana na Yanga, Namungo na Ruvu Shooting ambayo imetoka kutandikwa mabao 3-2 na Geita Gold
Ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 2-1 na Mtibwa kwenye mchezo uliopita, Kocha msaidizi wa Dodoma, Kassim Liyogope amesema wanaanza msako wa pointi 12 za nyumbani kwa kuikaribisha Ihefu na kuhitaji ushindi kwa lengo la kujiweka pazuri kwenye msimamo