Wakati uvumi ukienea kwamba Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi anawindwa kupewa kibarua cha kuwa kocha wa Timu ya Taifa 'Taifa Stars', mwenyewe ametoa hatma yake.
Nabi amesema kuwa anafurahia kupewa nafasi kubwa kama hiyo ya kuifundisha Taifa Stars lakini kwasasa ni vigumu kukubali ofa hiyo.
Nabi amesema kwasasa ajira pekee ambayo anaweza kuifanya akiwa ndani ya ardhi ya Tanzania ni kuendelea kuifundisha Yanga
"Nimeona hizo taarifa lakini hata familia yangu wameshtuka walipoona lakini niwashukuru wanaonifikiria kuhusu nafasi hiyo"
"Naomba waambie mashabiki wa Yanga kwamba mimi kwa hapa Tanzania kwasasa nitaifundisha timu yao pekee mpaka nitakapochukua uamuzi mwingine"
"Sina maana kwamba kuifundisha Tanzania ni kazi mbaya kwangu hapana lakini huwa nina utaratibu wa kumaliza jambo ambalo nimelianza," Nabi alinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
Tangu ajiunge na Yanga mwezi April 2021, Nabi ameisaidia timu hiyo kushinda mataji mawili ya ligi kuu na kombe la FA, Ngao mbili za jamii huku msimu huu akiiweka Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama nane
Huenda akawaongoza mabingwa hao watetezi kutetea ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo



