Kocha Msaidizi wa Geita Gold FC, Mathias Wandiba, amesema nguvu na akili zao wanazielekeza katika mchezo wa hatua ya 16 bora wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) maarufu FA Cup dhidi ya Green Warriors Ijumaa wiki hii
Mechi hiyo itapigwa uwanja wao wa nyumbani wa Nyakumbo, uliopo mkoani humo, wakiwakaribisha 'Wajeda' hao wa Ligi ya Championships, ambao maskani yao ni Dar es Salaam.
Wandiba alisema wamerejea nyumbani wakitokea Ruangwa baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC.
Alisema wanaendelea na maandalizi kwa kufanyia kazi madhaifu yaliyojitokeza katika mechi iliyopita na kujiimarisha kwa mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho la Azam.
"Maandalizi yanaendelea vizuri kwani ni mchezo uko kwenye ratiba kama ilivyo mechi zingine za ligi na wachezaji watakaokosekana kwa sasa hadi tupate ripoti ya daktari wa timu," alisema Wandiba.
Alisema hawana mpango wa kufanya mabadiliko ya kikosi katika mchezo huo na kwamba hilo linaweza kutokea endapo tu watapata ripoti ya daktari wa timu hiyo kutokana na kugundulika watawakosa baadhi ya wachezaji kwa sababu ya majeraha.