Wapinzani wa Simba katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Afrika, Vipers Fc kutoka nchini Uganda wanatarajia kuwasili nchini kesho Jumatatu Machi 6 ,2023 kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba utakaochezwa siku ya Jumanne ya Machi 7-2023 kwenye dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam
Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Simba Ahmed Ally amesema Vipers Fc wamethibitisha kuingia nchini mapema Jumatatu ambapo siku hiyo jioni watakuwa na ruksa ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Mkapa majira ya saa 1 usiku
Mgeni rasmi wa mchezo huo ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma
Simba inahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri katika mkakati wa kuisaka hatua ya robo fainali
Kimahesabu bado timu zote zina nafasi ya kusonga mbele hatua inayofuata katika kundi C pamoja na kuwa Raja Casablanca wao wana nafasi nzuri zaidi
Raja ndio vinara wa kundi C wakikusanya alama tisa baada ya kushinda mechi zote tatu wakati Horoya Ac inashika nafasi ya pili ikiwa na alama nne
Horoya wametofautiana alama moja tu na Simba iliyo nafasi ya tatu ikiwa na alama tatu. Vipers Fc wanaburuza mkia wakiwa na alama moja
Mechi za raundi ya nne zinaweza kutoa taswira ya nafasi ya Simba kuelekea robo fainali, lakini ushindi ndio matokeo pekee ambayo Simba inahitaji ili kuwa na matumaini