Rafinha aliihakikishia Fc Barcelona ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Valencia katika mchezo wa La Liga uliopigwa dimba la Camp Nou jana
Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Barca kuondoka na alama zote tatu wakilazimika kulinda bao moja wakiwa pungufu baada ya Ronald Araujo kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumfanyia madhambi Hugo Duro akiwa ni mlinzi wa mwisho
Barca wangeweza kumaliza mechi hiyo mapema kama Ferran Torres angefunga mkwaju wa penati mapema kwenye kipindi cha pili
Ushindi huo ulikuwa na thamani kubwa kwa Barca kwani wameendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa La Liga kwa tofauti ya alama tisa baada ya wapinzani wao Real Madrid kulazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Real Betis
Barcelona imefikisha alama 62 baada ya mechi 24 wakati Real Madrid wana alama 53 baada ya mechi 24 pia
Tangu ushindi wao wa mabao 5-2 dhidi ya Liverpool kwenye michuano ya ligi ya mabingwa, Real Madrid hawajafanikiwa kupata ushindi katika mechi tatu

Walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya mahasimu wao kutoka jiji la Madrid, Atletico kisha wakapoteza mchezo wa nusu fainali Copa Del rey dhidi ya wapinzani wao Barcelona kwa kufungwa bao 1-0 katika uwanja wao wa nyumbani na jana kulazimishwa suluhu dhidi ya Real Betis ugenini