Kocha Mkuu wa Simba Robertinho Oliveira amesema maandalizi kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Vipers Fc yamekamilika
Robertinho amesema wanatarajia mchezo utakuwa mgumu katika hatua hii lakini wao wanahitaji kutumia vyema uwanja wa nyumbani kushinda
"Tunatarajia mchezo mgumu siku ya kesho lakini sisi tumejipanga kwa ajili kutafuta ushindi. Katika hatua hii hakuna mchezo rahisi kila timu inashuka uwanjani kutafuta matokeo mazuri"
"Tumejiandaa vyema kucheza hapa nyumbani, tunafahamu ubora wa Vipers uko wapi hivyo tutakuwa makini hasa kwenye mashambulizi ya kushitukiza"
"Tayari nimeshaamua timu ambayo itashuka uwanjani kesho lakini siwezi kuweka hadharani hapa. Muhimu ni kuwa wachezaji wangu wako tayari, wana ari na morali kubwa kuelekea mchezo huo," alisema Robertinho
Nae nahodha Msaidizi wa Simba Shomari Kapombe amesema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo ambao wanahitaji kushinda
"Uzuri sisi kama wachezaji tunafahamu majukumu yetu, tunarejea katika uwanja wa nyumbani tukiwa na lengo moja tu kushinda. Tunajua katika mchezo uliopita hatukufanya vizuri lakini kesho tunarudi tukiwa imara na malengo makubwa ya ushindi"
"Tutafuata maelekeo ambayo Mwalimu ametuandalia kwa kuzingatia ubora wa Vipers Fc. Tumejiandaa vizuri kupata ushindi katika mchezo wa kesho lakini nawaomba mashabiki wa Simba waje kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa, wingi wao utatuongezea morali ya kupambana katika mchezo huo," alisema Kapombe