Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Real Bamako ambao utapigwa kesho Jumatano katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Nabi amesema wanahitaji kushinda mchezo huo pamoja na mchezo utakaofuata dhidi ya US Monastir ili kuwa na nafasi nzuri ya kutinga robo fainali
Nabi amesema mchezo wa mwisho ambao watacheza ugenini dhidi ya TP Mazembe utakuwa mgumu sana hivyo wanapaswa kutumia vyema uwanja wa nyumbani kukusanya alama sita katika mechi mbili za nyumbani wakianza na Real Bamako
"Tunacheza na timu ambayo tumetoka kucheza nayo Mali. Baada ya Bamako tutacheza na Monastir. Ni mechi ngumu lakini tunahitaji kushinda mechi hizi kwani mechi ya Mazembe itakuwa ngumu zaidi"
"Mechi dhidi ya Real Bamako itakuwa ngumu lakini tumejiandaa, tuko vizuri tutapambana ili tupate ushindi"
"Wachezaji hata sisi makocha hatukufurahia matokeo tuliyopata Mali, tuliumia Real Bamako kusawazisha dakika za mwisho, wachezaji wameahidi kupambana kupata ushindi mnono hapo kesho"
"Tunafahamu Real Bamako hawakuja kufanya utani hivyo tunajua mechi itakuwa ngumu lakini tutajitahidi tupate ushindi," alisema Nabi
Nabi alibainisha kuwa winga Jesus Moloko alipata majeraha kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons, atafanyiwa tathmini ya mwisho baada ya mazoezi ya leo
"Pia tunasikitika kumkosa Salum Abubakar ambaye amefiwa na mtoto wake leo," alisema Nabi
Aidha Nabi amesema wamefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mechi zilizopita hasa kwenye mipira ya kona
"Ni kukosa umakini na wachezaji kutokuwa na mawasiliano imepelekea kuruhusu mabao manne ya aina moja katika mechi zilizopita. Jambo hili halihusiani na vimo vya wachezaji, tumefanyia kazi, naamini wachezaji wangu wataongeza umakini katika kukabiliana na mipira inayotokana na kona au faulo"