Baada ya kiungo Casemiro kuoneshwa kadi nyekundu kwa mara pili ndani ya wiki kadhaa kwenye Ligi kuu England na kufungiwa kucheza mechi 4 Klabu ya Manchester United imeamua kuwa haitakata rufaa dhidi ya adhabu hiyo.
Casemiro alioneshwa kadi nyekundu katika mchezo wa sare ya 0-0 dhidi ya Southampton katika dimba la Old Trafford siku ya Jumapili ikiwa ni takribani mwezi mmoja tu tangu aoneshwe kadi nyekundu baada ya kumkaba koo mchezaji wa Crystal Palace katika ushindi wa 2-1 mnamo Februari 4, 2023.
Mwamuzi wa mchezo wa Jumapili Anthony Taylor awali alimuonesha Casemiro kadi ya njano baada ya rafu mbaya lakini VAR iliingilia kati na kumtaka Taylor abadili maamuzi kabla ya kufuta kadi ya njano na kumlima kadi nyekundu.
Mashetani Wekundu wanaamini kulikuwa na uwezekano mdogo wa uamuzi huo kubatilishwa na sasa Mbrazil huyo atatumikia adhabu ya kutocheza mechi nne zinazoandaliwa na Chama cha Soka England FA).
Casemiro atakuwa nje ya mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Fulham na michezo ya Ligi Kuu dhidi ya Newcastle United, Brentford na Everton.
"Casemiro amecheza zaidi ya mechi 500 Ulaya hakuwahi kuoneshwa kadi nyekundu lakini sasa tayari ana kadi mbili nyekundu kwenye Ligi kuu England," alisema Meneja Erik ten Hag baada ya mechi dhidi ya Southampton



