Kikosi cha Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), kitaondoka nchini kwa makundi kuelekea Misri kwa ajili ya kuweka kambi maalumu ya kujiandaa kuwakabili Uganda (Cranes), katika mechi ya kwanza ya kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Afrika (AFCON)
Uganda itawaalika Taifa Stars Machi 24, mwaka huu katika mji wa Ismailia, Misri na timu hizo zitarudiana Machi 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa TFF, Clliford Ndimbo, alisema jana kikosi cha Stars kitasafiri kwa awamu mbili na hiyo imetokana na timu za Simba na Yanga kukabiliwa na mechi za mashindano ya CAF.
"Kikosi cha Stars kinatarajia kuondoka katika makundi mawili kuelekea Misri, kundi la kwanza litaondoka Machi 16 na la pili Machi 20, kwenda kuweka kambi huko Misri, tumefanya hivyo kwa sababu kuna timu zinakabiliwa na mashindano ya CAF, kwa maana ya Simba na Yanga"
"Tunatazama mchezo huu kwa umakini mkubwa, nia ni kuona tunafanikiwa kuingia katika mashindano ya AFCON 2023, kwa mara ya tatu, ndio maana tunahakikisha kila kitu kinakaa sawa," alisema Ndimbo.
Aliongeza benchi la ufundi limejipanga kuhakikisha wanafikia malengo ya kufuzu fainali hizo za AFCON kwa mara nyingine.
Mara ya mwisho Taifa Stars ilishiriki fainali za AFCON mwaka 2019, ambazo zilifanyika Misri, iliongozwa na Mnigeria, Emmanue Amunike.